MASOMO YA MISA, MEI 08, 2023
JUMATATU, JUMA LA 5 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 14:5-18
Siku zile, palipotokea shambulio la watu wa
Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga
kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, mji wa Likaonia, na
nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra
palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye
hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia
macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa
miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.
Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo
wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya
wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa
mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta
ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na
makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo
zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina
bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi ni wanadamu hali moja na ninyi;
twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na
kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote
vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia
zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema,
akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu
chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida,
wasiwatolee dhabihu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 115 :1-4, 15-16 (K) 1
(K) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali
ulitukuze jina lako.
Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi,
Bali ulitukuze jina lako.
Kwa ajili ya fadhili zako,
Kwa ajili ya uaminifu wako.
Kwa nini mataifa kusema,
Yuko wapi Mungu wao? (K)
Lakini Mungu wctu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu. (K)
Na mbarikiwe ninyi na Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
Mbingu ni mbingu za Bwana,
Bali nchi amewapa wanadamu. (K)
SHANGILIO
Col. 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI
Yn. 14:21-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Yeye aliye na
amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na
Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote),
akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa
ulimwengu?
Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda,
atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya
makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno
mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo
niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho
Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na
kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment