MASOMO YA MISA, APRILI 30, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 13:13-25
Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri
kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohane akawaacha akarejea
Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika
Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.
Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma
mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa
lisemeni.
Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema,
Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli
aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni
katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.na kwa
muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa. Na alipokwisha
kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa
muda wa miaka kama mia nne na hamsini; baada ya hayo akawapa waamuzi hata
zamani za nabii Samweli. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli
mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini. Na
alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia,
akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu,
atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli
Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri
watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye
Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi
siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sisitahili
kumlegezea viatu vya miguu yake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 89:1-2, 20-21, 26-27 (K) 1
(K) Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele.
Kwa kinywa change
Nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, FAdhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)
Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
Na mkono wangu utamtia nguvu. (K)
Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya.
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua,
wao wanifuata.
Aleluya.
INJILI
Yn. 13:16-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin,
nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko
yeye aliyempeleka.
Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. Sisemi
habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate
kutimizwa, aliyekula chakula change ameniinulia kisigino chake.
Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili
yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye. Amin, amin, nawaambieni, Yeye
ampokeaye mtu yeyote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea
yaye aliyenipeleka.
Neno la Bwana… Sifa kwako Eee Kristo.
Copyright © 2026, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment