MASOMO YA MISA, MEI 14, 2025
JUMATANO YA 4 YA PASAKA
SIKUKUU YA MT. MATHIA, MTUME
SOMO 1
Mdo. 1:15-17, 20-26
Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake
(jumala ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko
litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi. katika
habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa
amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa
katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa,
Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena,
Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote
Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane,
hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa
kufufuka kwake pamoja nasi.
Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba,
aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe,
Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa
wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende
zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye
akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.
W1MBO WA KATI KATI
Zab. 113:1-8 (K) 8
(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu
wa watu wake. au: Aleluya.
Aleluya.
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele. (K)
Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)
Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani? (K)
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
Amketishe pamoja na wakuu,
Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)
SHANGILIO
Yn. 15 :16
Aleluya, aleluya, Ni mimi niliyewachagua ninyi,
nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa. Aleluya.
INJILI
Yn. 15:9-17
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba
alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.
Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika
amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha
yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.
Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama
nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa
uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda
niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake;
lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu
nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba
lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate
kupendana.
Neno la Bwana.........Sifa kwako Ee
Kristo.
Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment