MASOMO YA MISA, MEI 11, 2025
JUMAPILI YA 4 YA PASAKA, MWAKA C
JUMAPILI YA MCHUNGAJI MWEMA
SIKU YA KUOMBEA MIITO
MWANZO:
Zab. 33:5-6
Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana
mbingu zilifanyika, aleluya.
SOMO 1
Mdo 13:14, 43-52
Paulo na Barnaba walitoka Perge, wakapita kati
ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya
sabato, wakaketi. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi
wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu
katika neema ya Mungu.
Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji
wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona
makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na
kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno
la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona
nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.
Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana.
Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa
wokovu hata mwisho wa dunia.
Mataifa waliposikia hayo wakafurahi,
wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele
wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.
Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa
wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba;
wakawatoa katika mipaka yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na
Roho Mtakatifu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 100:1-3,5 (K) 3
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)
Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SOMO 2
Ufu. 7:9, 14b-17
Wakati ule, mimi, Yohane, niliona, na tazama,
mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na
kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za
Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.
Mmoja wa wale wazee akiniambia, Hao ndio
wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe
katika damu ya Mwana-kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha mungu,
nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika
kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona
kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo
Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza
kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho
yao.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu
nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 10:27-30
Yesu alisema; Kondoo wangu waisikia sauti yangu;
nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea
kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu
aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika
mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment