MASOMO YA MISA, APRILI 19, 2024
IJUMAA, JUMA LA 3 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 9:1-20
Siku zile, Sauli, akizidi kutisha na kuwaza
kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kwenda
Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa
wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.
Hapo alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia
Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini,
akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe,
Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie
mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye
wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka katika nchi, na
macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka
Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
Basi palipokuwapo Dameski mwanafunzi jina lake
Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana
akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika
nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye
amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate
kuona tena.
Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari
za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako
Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote
wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maan ahuyu ni
chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na
wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa
ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani, akamwekea
mikono akisema, Ndugu, Sauli, Bwana amenituma, Yesu yeye aliyekutokea katika
njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka
machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa, akala
chakula, na kupata nguvu.
Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na
wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye
ni Mwana wa Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117 (K) Mk. 16:15
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini. (K)
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO
Rum. 6:9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena,
wala mauti haimtawali tena. Aleluya.
INJILI
Yn. 6:52-59
Siku ile, Wayahudi walishindana wao kwa wao
wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?
Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni,
Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani
yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami
nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu
yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa
ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi,
nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho
chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali
akilaye chakula hicho ataishi milele.
Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa
akifundisha, huko Kapernaumu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment