MASOMO YA MISA, MEI 12, 2023
IJUMAA, JUMA LA 5 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 15 : 22-31
Siku zile, baada ya Mtaguso wa Yerusalemu,
ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na
kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa
Barnaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu.
Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, Mitume
na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa
Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua
kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona
vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu
pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatirisha maisha yao kwa
ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila,
watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza
Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo valiyo lazima, yaani,
mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama
zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu.
Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia
Antiokia; na baada ya kuwakusanyia jamii yote wakawapa ile barua. Nao
walipokwisha kuisoma, wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA K.ATIK.ATI
Zab. 57 : 7-11 (K) 9
(K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
au: Aleluya.
Ee Mungu, moyo wangu u thabiti,
Moyo wangu u thabiti.
Nitaimba, nitaimba zaburi,
Amka, utukufu wangu.
Amka, kinanda na kinubi,
Nitaamka alfajiri. (K)
Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,
Na uaminifu wako hata mawinguni.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua,
nao wanifuata.
Aleluya.
INJILI
Yn. 15 :12-17
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amri
yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo
mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda
niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake;
lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu
nimewaarifu.
Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu
yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya
nawaamuru ninyi, mpate kupendana.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment