“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
JUMATATU, JUMA LA 3 LA PASAKA
APRILI 15, 2024
KUKUTANA NA MCHUNGAJI MWEMA ANAYETAKATISHA ROHO ZETU
Shangwe za Pasaka zinaendelea kutupa msingi hasa tunapo ingia katika juma la tatu la Pasaka. Mchungaji mwema amefufuka. Yeye ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake, amefufuka. Yeye ambaye anatupenda na kulinda kundi lake hakuweza kufungwa na kifo. Kilicho cha muhimu anaendelea kuwa mchungaji wetu mwema.
Shemasi Stefano alifanya kazi muhimu sana katika kanisa la mwanzo. Maisha yake ya kujitoa kabisa kwa Yesu, utayari wake wa kufa kwa ajili yake, Stefano anakuwa mfano kwa Wafiadini wote waliokuja baadae, na hata kwa wakristo wote wa nyakati zote. Leo tutasikia yupo katika kujaribiwa na kesho tutasikia kuuwawa kwake. “Wana heri ambao maisha yao hayana hatia”.
Mafundisho ya Yesu leo ni muhimu sana katika kuelewa kwetu juu ya asili ya Ekaristi na jinsi anavyotaka sisi tuijongee. Kundi lile ambalo lililishwa kwa mikate na samaki wawili sasa wapo katika kumtafuta. Kumtafuta Yesu ni muhimu sana, lakini cha muhimu yule mtafutaji lazima atambue nia yake mathubuti. Yesu anawambia, “hakika nawaambia hamnitafuti mimi kwasababu mliona miujiza, lakini kwasababu mlikula mikate na kushiba”.
Kumtafuta huku hakukuwa kwasababu ya upendo kwake, bali kufaidika naye. Sisi mara nyingi tunamtafuta Yesu kwa faida zetu, pengine kwasababu ya gari, nyumba, mchumba mwema, kuponywa kutoka katika magonjwa. Yesu aliwaonya watu wasitafute vitu viharibikavyo bali vya milele (Yesu mwenyewe). Tatizo ni hili sisi kama lile kundi, hatumtafuti Yesu zaidi ya chakula na mahitaji ya kimwili, hatumtambui kwamba yeye anafanya mioyo yetu safi kwa chakula cha milele anachotupa.
Yesu anaendelea kuwa mchungaji wetu mwema sasa. Anafanya hivi kwakutufundisha ni kitu gani tunachohitaji hasa kwa ajili ya maisha yetu, ambacho ni Ekaristi. Ni sakramenti kubwa kuliko zote, ambayo tunapaswa kuwa tumejiandaa, ili tuweze kukutana na Yesu mfufuka.
Sala: Mungu Baba yetu mwanga wako wa ukweli unatuangaza kwenye njia za Yesu Kristo. Bwana tunakuomba utuimarishe kwa sakramenti hii ya Ekaristi, ili tuweze kupata Amani, upendo, na kumjali Yesu Mchungaji wetu mwema.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment