MASOMO YA MISA, JUMAPILI, APRILI 20, 2025
DOMINIKA YA PASAKA
MWANZO:
Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umweniwekea
mkono wako,
maarifa hayo ni ya ajabu, aleluya.
SOMO 1
Mdo. 10:34, 37- 43
Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo
lile ninyi mmelijua, lilionea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya
ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia
mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi
njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu aikuwa pamoja
naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote yaliyotendeka katika nchi ya Wayahudi na
katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua
siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi
waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndiyo sisi, tuliokula na kunywa naye
baada ya ufufuka kwake kutoka kwa wafu. akatuagiza tuwahubiri watu na
kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe mhukumu wa wahai na
wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye
atapata ondoleo la dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI.
Zab. 118:1-2, 16-17, 22-23.
K. Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia.
Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele. (K)
Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)
Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la Pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu (K)
SOMO 2
Kol. 3:1-4
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo
juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja
na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi
mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Aleluya Aleluya!
Kristo, Paska wetu amekwisha kutolewa sadaka;
Basi natuifanye karamu katika Bwana!
Aleluya
INJILI
Yn. 20:1-9.
Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu
Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe
limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule
mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana
kaburuni, wala hatujui walipomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi
mwingine , wakashika njia kwenda kaburini wakaenda mbio wote wawili; na yule
mwanafunzi wengine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika
kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini
hakuingia. Basi akaja Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi;
akavitazama vitambaa vilivyolala; ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala
pamoja na vitambaa, bali imezogwazogwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo
alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika
kaburini, akaona na kuamini. kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba
imempasa kufufuka.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment