MASOMO YA MISA, APRILI 5, 2025
SOMO 1
Yer. 11:18-20
Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo
uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole,
achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu,
wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke
katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.
Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki
ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana
nimekufunulia wewe neno langu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 7:1-2, 8-12 (K) 1
(K) Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.
Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama samba,
Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya. (K)
Bwana, unihukumu mimi,
Kwa kadiri ya haki yangu,
Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome,
Lakini umthibitishe mwenye haki. (K)
Ngao yangu ina Mungu,
Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)
SHANGILIO
Lk. 15:18
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na
kumwambia: Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.
INJILI
Yn. 7:40-52
Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya
Yesu, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye
Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya
kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa
Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao
wakataka kumkamata, alkini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.
Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa
makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi
wakajibu, Hajanena kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo
wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au
katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa.
Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea
zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia
kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka
Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment