MASOMO YA MISA, APRILI 16, 2025
JUMATANO YA JUMA KUU
SOMO 1
Isa 50:4-9a
Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao,
nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi
baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.
Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea
wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu
usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu
hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua
ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani
atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na
anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa
mkosa?
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab 69:7-9, 20-21, 30, 32-33
(K)Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.
Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu,
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu. (K)
Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana.
Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.
Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. (K)
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafungwa wake. (K)
INJILI
Mt 26:14-25
Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake
Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa,
nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati
huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate
isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo
tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie,
Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na
wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa
Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao
walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.
Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu
akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye
atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole
wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama
asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi?
Akamwambia, Wewe umesema.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment