MASOMO YA MISA JANUARI 25,
2024
IJUMAA, JUMA LA 2 LA MWAKA
SIKUKUU YA KUONGOKA KWA MT.
PAULO, MTUME
SOMO 1
Mdo 22:3-16
Paulo aliwaambia makutano,
Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa
katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa
usahihi nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi
watu wa njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani wanaume na
wanawake. Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia,
ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili
niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
Ikawa nilipokuwa nikisafiri,
nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni,
ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli,
Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu
Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami, waliiona ile
nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie
Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na
nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao
waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.
Basi mtu mmoja, Anania,
mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,
akanijia, akasimama karibu nami akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone.
Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua
wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti
itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa
mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa unakawilia nini? Simama,
ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117:1-2 (K) Mk. 16:15
(K) Enendeni ulimwenguni
mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aleluya!
Enyi mataifa yote, msifuni
Bwana,
enyi watu wote, mhimidini.
(K)
Maana fadhili zake kwetu sisi
ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa
milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:16
Aleluya, aleluya,
Niliwachagua ninyi,
nikawaweka mwende mkazae matunda,
matunda yenu yapate kukaa.
matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya.
INJILI
Mk. 16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi
na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila
kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Maana ishara
hizi zintafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa
lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru
kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Neno la Bwana… Sifa kwako ee
Kristo.
Copyright © 2024,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
Amina, hongera kwa kazi nzuri
ReplyDelete