Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 14, 2024





MASOMO YA MISA, NOVEMBA 14, 2024
ALHAMISI, JUMA LA 32 LA MWAKA

SOMO 1
Flm. 7 – 20

Nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.
Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasako; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moy wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili.

Lakini sikutaka kutenda neno lolote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike ndicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 146:7 – 10 (K) 5

(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.

Bwana huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula,
Hufungua waliofungwa. (K)

Bwana huwafumbua macho walopofuka,
Bwana huwainua walioinama,
Bwana huwapenda wenye haki,
Huwahifadhi wageni. (K)

Huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi.
Aleluya. (K)


SHANGILIO
Zab. 27:11

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, uifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.


INJILI
Lk. 17:20-25

Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.

Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment