MASOMO YA MISA OKTOBA 27, 2024
JUMAPILI YA 30 MWAKA B
SOMO 1
Yer. 31:7-9
Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke wmenye mimba, nay eye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K)
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)
Ndipo mataifa waliposema,
Bwana amewatendea mambo makuu,
Bwana alitutendea mambo amkuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee, Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
SOMO 2
Ebr. 5:1-6
Ndugu, kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ilia toe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Ef. 1:17-18
Aleluya, aleluya,
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uyatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.
INJILI
Mk. 10:46-52
Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, Imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
🙏🙏🙏🙏
ReplyDelete🙏🙏
ReplyDeleteAmina
ReplyDeleteAmen
ReplyDelete