“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Septemba 22, 2024.
Dominika ya 25 ya Mwaka B wa Kanisa
Hek 2: 12, 17-20;
Zab 53: 3-6, 8;
Yak 3: 16- 4:3;
Mk 9: 30-37.
NI NANI ALIYE MKUBWA?
Katika Injili ya leo tunawaona mitume wakihojiana kuhusu swali hili. Yesu hajafurahishwa na kitendo hiki. Hakutaka kuona wivu na tamaa za uongo kutoka kwao. Alitaka wao waishi kwa Amani na upendo.
Patrick alikuwa Daktari. Mtu wa heshima yake, kiongozi wa jumuiya. Alikuwa na hela nyingi. Alikuwa na gari zuri na pia nyumba zuri. Lakini alikuwa anachagua watu wake wa kusalimia na kuongea nao.
Kwa upande mwingine Joseph alikuwa ni baba wa watoto tisa. Alikuwa na nyumba ya hali ya chini. Lakini nyumbani kwake palikuwa ni sehemu ya watu kukutana na wakati mwingine kubadilishana mawazo na kila mtu alijisikia huru kwenda katika nyumba yake na kuongea naye na hata wakati mwingine wengine kulikutana kwake bila uwepo wake. Joseph alikuwa ni mtu mwenye furaha daima alikuwa tayari kumpa mtu mkono na kumsalimia. Alipofanya kazi kila mtu alimpenda kwa uchangamfu wake wa kucheka na kila mtu na watu walimpenda. Hakuwa na elimu kubwa lakini alijielewa na jinsi ya kuwa Baba mwema wa familia. Alikuwa rafiki kwa kila mtu na alikuwa akifanya kazi ya ulinzi tena kulinda mlango wa kuingia shuleni.
Sifa za Patrick sio nyingi kama za Joseph. Haya ndio mambo tunayofanya kila siku. Pengine huwa tunawaona watu katika mtazamo wa kazi zao kwanza. Tunaangalia kazi ya mtu kwanza alafu utu wake unakuja baadae. Je, ni kipi kilicho na maana kwanza, utu wa mtu au kazi ya mtu? Ni utu wa mtu unapaswa kuja kwanza na wala si kuangalia kazi yake.
Tukigeukia injili tunaona kwamba hili lilikuwa likifanana na kosa walilotenda mitume. Kwao ilikuwa ni kazi, na madaraka ndicho kilichokuwa muhimu. Kwao, mtu mkubwa ni yule aliyekuwa na madaraka makubwa, ambaye anafuata tu baada ya Bwana wao. Na kila mmoja anataka kupata nafasi hiyo, bila sababu ya maana. Walikumbwa na wivu na ubinafsi. Walikuwa na mawazo ya kudhani kwamba Yesu ataingia katika madaraka ya kiulimwengu zaidi na utukufu wa kiulimwengu.
Yesu anawarekebisha na kuwarudisha katika mstari mzuri. Ufalme wake sio shauri la kutafuta madaraka na utukufu binafsi. Bali ni kwa ajili ya kuwatumikia wengine. Kama watakuwa tayari kuwatumikia wengine ni wazi kwamba watakuwa na nafasi ya kwanza. Na hivyo sio kukaa katika viti vya juu na wengine kupita mbele yao na kuwasujudia. Badala yake wanapaswa kupiga magoti na huku wakiwa wamebeba beseni la maji na taulo upande huu tena wakiosha miguu ya wadogo. Kama wapo tayari kwa hali ya namna hii watakuwa tayari kukaribishwa katika hali ya juu.
Sio kile tunachofanya kilicho cha muhimu-kuwa daktari, seremala au dereva. Badala yake mimi ni daktari wa namna gani? Mimi ni seremala wa namna gani, mimi ni dereva wa namna gani? Sio nini ninafanya bali mimi ni wa namna gani ndicho kilicho cha muhimu. Yesu hakuongea tu ili sisi tufanye, yeye mwenyewe alionesha mfano kamili. Yeye alijitoa sadaka kwa ajili yetu. Hakuna mtu ambaye anaweza kufanya katika hali ya juu kama Yesu. Yeye ni mkuu kweli kweli lakini kama alivyo ahidi tukimwamini tutafanya makuu hata kuliko yeye mwenyewe.
Kitu kingine kwenye injili ni picha ya mtoto ambayo anaitumia Yesu kuweza kusisitiza ujumbe wake. Hapa tunapaswa kuchukulia mtu ambaye ana moyo kama wa mtoto, mnyoofu tofauti na mtu yule ambaye hutegemea ukuu wa dunia kwa kutazama wingi wa mali zake. Mtoto ni mtu ambaye ni maskini, anategemea wazazi, mnyoofu na mhitaji. Mtoto hawezi kujitegemea mahitaji yake. Badala yake mtoto anahitaji matunzo kutoka kwa wazazi wake. Hivi ndivyo tunavyopaswa kuwa, uhusiano wetu na Mungu unapaswa kuwa wa namna hii. Hatuwezi kuhesabiwa kuwa wakuu kwa kujitenga na kufanya mambo yetu peke yetu, au kwa kufanikiwa kuwa na mali nyingi bila kujali wengine. Hali hii ni hali ya kiulimwengu kuhusu kuwa mkuu. Ukuu hautokani na mali ulizopata bali unatokana na kumtegemea Kristo. Na pia unapatikana kwa kuwatafuta wale waliowahitaji na kuwasaidia. Ni wito wa kuwa na huruma kwa maskini na wahitaji.
Tafakari leo kama upo tayari kuwatembelea wale walio wahitaji na kuwafariji. Je, unawatafuta na kutaka kuwatumikia na kuwasaidia? Kwakufanya hivi, hili ndilo litakalo kufanya mkuu mbele ya macho ya Mungu.
Sala: Bwana, ninakuomba nikutafute wewe kwa maskini, wale waliopondeka moyo, wadhambi na wale walio wahitaji. Ninakuomba ujaze moyo wangu na huruma na majitoleo kwa wengine. Yesu, nakuamini wewe. Amina
.Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
Amina
ReplyDelete