Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 22, 2024



MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 22, 2024
DOMINIKA YA 25 YA MWAKA B


MWANZO:
Bwana asema: Mimi ni wokovu wa watu. Wakinililia katika taabu yoyote nitawasikiliza, nami nitakuwa Bwana wao milele.


SOMO 1
Hek. 2:12:17-20

Zaidi ya hayo tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu, atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 54:1-4, 6 (K) 4

(K) Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.

Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe,
Na kwa uwezo wako unifanyie hukumu.
Ee Mungu uyasikie maombi yangu,
Uyasikilize maneno ya kinywa changu. (K)

Kwa maana wageni wamenishambulia,
Wote watishao wanaitafuta nafsi yangu;
Hawakumweka Mungu mbele yao. (K)

Tazama, Mungu anayenisaidia;
Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu.
Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu,
Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema. (K)


SOMO 2
Yak. 3:16-4:3

Hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki, na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani. Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yetu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Mdo. 16:14

Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.


INJILI
Mk. 9:30-37

Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.
Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njia walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi, na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

3 comments: