Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, AGOSTI 18, 2024



MASOMO YA MISA, AGOSTI 18, 2024
DOMINIKA YA 20 YA MWAKA B

SOMO 1
Mit 9:1-6

Hekima ameijenga nyumba yake, amezichonga nguzo zake saba; Amechinja nyama zake, amechanganya divai yake, ameiandalia meza yake pia. Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana, Kila aliye mjinga na aingie humu, Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya. Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 34:1-2, 9-14 (K) 8

(K) Onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema.

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
wanyenyekevu wasikie wakafurahi. (K)

Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake,
Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
Wana-sifmba hutindikiwa, huona njaa;
Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu
Chochote kilicho chema. (K)

Njoni, enyi wana, mnisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Bwana.
Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima,
apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)

Uuzuie ulimi wako na mabaya,
Na midomo yako na kusema hila.
Uache mabaya ukatende mema,
Utafute amani ukaifuatie. (K)


SOMO 2
Efe 5:15-20

Angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Yn 14:6

Aleluya, aleluya,
mimi ndimi Njia, na Ukweli, na Uzima, asema Bwana; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.


INJILI
Yn 6:51-59

Yesu aliwaambia makutano: Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

1 comment:

  1. aulaye mwili wangu na kuinywa damu ungu,hukaa ndani yangu nami ndani yake...mbarikiwe sana watumishi wa mungu ...Amina

    ReplyDelete