“MBEGU ZA UZIMA”
Julai 14, 2024
Dominika ya 15 ya Mwaka
Amo 7:12-15;
Zab 85:8-13;
Efe 1:3-14;
Mk 6:7-13.
UJUMBE WA MUNGU NYAKATI ZA KUKATALIWA NA KUTESWA
Yesu alikaa pamoja nasi, akifanya miujiza na kutupa neno lake. Lakini hata hivyo watu walipenda mafundisho na miujiza yake kwa faida zao za kibinafsi tu. Hawakua na nia ya kumfanya huyu Yesu kuwa mfano wa kuiga. Hawakutaka kuwa kama Yeye. Je, ungekuwa na Imani ya kufanya mafundisho ya Yesu yakubadilishe na kukufanya wewe kuwa kama Yeye? Au labda ungekuwa unaishi kwa mashaka naye na dharau kama walivyokuwa watu wa Nazareti ambao tunawasikia katika injili ya leo? Yesu anaendelea kufanya utume wake leo kati yetu, akituponya na kutufundisha, lakini hata hivyo bado kuna watu hawana Imani na Yesu, ya kumfanya aendelee kufanya miujiza na kuwafundisha kupitia Kanisa lake.
Katika somo la kwanza tunasikia Mungu akimuita nabii Amosi na kumtuma aende kunena na taifa la Israeli lililopotoka. Mt. Paulo daima alikuwa katika majibizano makali na waliojiita wa Yudea. Hawa walikuwa ni wakristo kutoka jamii ya Kiyahudi, ambao waliwataka watu wa mataifa wawe Wayahudi kwanza na kushika sheria zao kabla ya kuwa wakristo. Kundi lingine lililokuwa kinyume na Paulo ni lile aliloliita walimu wa uongo. Hawa walidai kumiiliki muongozo wa pekee uliotolewa kwa wachache walioteuliwa tu. Ndipo Paulo akasimama na kuihubiri Injili iliyotolewa bure kwa wote. Katika mitafaruku kama hii, Paulo hakuwa mtu wa kukubali kushindwa kirahisi. Paulo anawatia moyo wasomaji wake waweze kusafiri ile njia kuu pamoja nae kwa kuwaonesha jinsi Mungu alivyo wahusisha wao katika mpango wake wa mwisho na wa milele kwa ulimwengu wote. Anaianza barua yake kwa kanisa la Efeso kwa maneno mazito na ya furaha akisifu na kusema, “Atukuzwe Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aliyetubariki kwa kila Baraka za rohoni kutoka Mbinguni”
Katika injili ya leo, Yesu anakataliwa na watu wa nchi yake
(Mk.6:1-5) na anaitikiwa kama ifuatavyo:
(Mk.6:1-5) na anaitikiwa kama ifuatavyo:
1. Yesu anaondoka na kuelekea vijiji vya jirani (Mk.6:6)
2. Anapanua wigo wa utume wake kwa kuwatangazia Habari njema watu wengine na kuwaweka katika mpango wake. Anawakusanya mitume kumi na mbili na kuwatuma wawili wawili, kuwapa mamlaka juu ya roho chafu.
Mpango wa Mungu Bila Kujali Muitikio.
Nia ya Mpango wa Mungu ni rahisi na Mkubwa mno. Wafuasi hawawezi kwenda wenyewe bali wawili wawili, ikimaanisha jimuiya, na upendo kati ya mtu na mtu. Wanapokea mamlaka juu ya roho chafu, ili kuwasaidia wanaoteseka na kuwaandaa kupata muunganiko na Mungu.
Ujumbe wa Mungu Kwa Watu
Wafuasi walipokea miongozo mingi ambayo iliwasaidia kuelewa muelekeo sahihi wa mpango wa kutangaza Habari njema waliyoipokea kwaYesu.
a) Wanapaswa kutokuwa na chochote, wala fedha wala fimbo, wala mkate, wala viatu, wala kanzu mbili. Hii inamaanisha kwamba Yesu anawataka wategemee ukarimu wa watu. Kwakuwa aendaye bila kitu atapokelewa vyema.
b) Wanapaswa kula walichokula watu au walichopewa. Hii inamaanisha kwamba katika kukutana na watu wasijali kuvunja sheria za utakaso kama zilivyofundishwa enzi zile.
c) Wanapaswa kukaa katika nyumba ya kwanza waliyokaribishwa. Wanapaswa kukaa pamoja na wasiende nyumba hadi nyumba, kwa maneno mengine wanapaswa kushiriki katika maisha na kazi za watu wengine na watu wangewapokea katika jumuiya na kushiriki katika chakula pamopja nao.
d) Wanapaswa kuwahudumia wagonjwa, kuwaponya waliopooza na kutoa mapepo. Walitakiwa kuikusanya jamii ilioyotawanyika na kuleta roho ya maisha ya jumuiya kati yao, ambamo upendo utawakumbatia wote bila kujali wagonjwa, au waliopagawa na pepo na kupitia upendo wa Mungu wapate uponyaji na wokovu. Ufalme wa Mungu unakuja na unakuwa hai pale ambapo watu kupitia Imani, wataamua kuishi kijumuiya kutoa ushuhuda na wadhihirisha kwa wote kuwa Mungu ni Baba na hivyo sisi binadamu ni kaka na dada.
Kama ambavyo Mungu alimuita Amosi Na Paulo na kuwaambia wapeleke ujumbe wake katika uso wa machafulo, ndivyo Yesu alivyokataliwa na kuwaandaa wafuasi wake pia kukataliwa. Leo kanisa linapitia Mateso, kukataliwa na kutokuelewana, lakini hata hivyo linaendelea kuhubiri na kufanya utume wake katika Jina la Yesu kwasababu kanisa limeitwa kufanya utume wa Yesu, bila kujali kukubaliwa au kukataliwa. Kama watu wangetambua hili, bila shaka wangeelewa kwamba, mafundisho ya kanisa yapo ili kujenga utawala wa Mungu mashani mwao. Na kuwaletea Kila Baraka za rohoni zilizoandaliwa kwa ajili ya watu wote.
Sala: Bwana, niimarishe mimi katika utume wangu kuhubiri ujumbe wako.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment