Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 14, 2024



MASOMO YA MISA, JULAI 14, 2024
JUMAPILI YA 15 YA MWAKA B


Somo 1
Amo 7:12-15

Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.

Neno la Bwana.........Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI

Zab 85:8-13

Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA,
Maana atawaambia watu wake amani, 
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K)Ee Bwana utuonyeshe rehema zako utupe wokovu wako.

Fadhili na kweli zimekutana, 
Haki na amani zimehusiana.
Kweli imechipuka katika nchi, 
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K).

Naam, Bwana atatoa kilicho chema, 
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake, 
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K).


Somo 2
Efe.1:3-14

Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.

Neno la Bwana.......tumshukuru Mungu.


Shangilio
Yn 1:12,14

Aleluya, aleluya
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; 
Wote waliompokea aliwapa uwezo 
wa kufanyika watoto wa Mungu. 
Aleluya


Injili
Mk 6:7-13

Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

Neno la Bwana...........sifa kwako Ee Krist0.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment