Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 17, 2024




MASOMO YA MISA, JULAI 17, 2024
JUMATANO YA 15 YA MWAKA


SOMO 1
Isa. 10: 5 – 7, 13 – 16

Bwana asema hivi: Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.

Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; name nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa maji za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia.

Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti.

Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapekelea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 94: 5 – 10, 14 – 15 (K) 14

(K) Bwana hatawatupa watu wake.

Ee Bwana, wanawaseta watu wako;
Wanauseta urithi wako;
Wanamwua mjane na mgeni;
Wanawafisha yatima. (K)

Nao husema, Bwana haoni;
Mungu wa Yakobo hafikiri.
Enyi wajinga miongoni mwa watu fikirini;
Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? (K)

Aliyelitia sikio mahali pake asisikie?
Aliyelifanya jicho asilione?
Awaadhibuye mataifa asikemee?
Amfundishaye mwanadamu asijue? (K)

Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake.
Wala hutauacha urithi wake,
Maana hukumu itairejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)



SHANGILIO
Zab. 27:11

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.



INJILI
Mt. 11:25 – 27

Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yenyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment