MASOMO YA MISA, JUNI 1, 2024
JUMAMOSI, JUMA LA 8 LA MWAKA
SOMO 1
Yud. 17:20-25
Wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.
Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu; Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 63:1-5 (K) 1
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.
Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. (K)
Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu. (K)
Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. (K)
INJILI
Mk. 11:27-33
Yesu na wanafunzi walifika Yerusalemu; alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya? Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. Ubatizo wa Yohane ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni.
Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu. Waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohane kuwa nabii halisi. Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment