MASOMO YA MISA, JUNI 15, 2026
JUMATATU, JUMA LA 11 LA MWAKA
SOMO 1
1 Fal. 21:1-16
Nabothi Myezreeli alikuwa na
shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme
wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu
nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa
badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha
sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe urithi
wa baba zangu.
Basi Ahabu akaenda nyumbani
kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na
Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani
pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli mkewe akamwendea,
akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? Akamwambia, Kwa
sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la
mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake.
Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu.
Yezebeli mkewe akamwambia, Je!
Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi;
mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.
Basi, akaandika nyaraka kwa
jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa
watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi.
Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkaweke
Nabothi juu mbele ya watu; mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki,
na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje,
mkampige kwa mawe, ili afe.
Wale wazee wa mji wake, na
walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza,
kama ailivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu
kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu
wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia
Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo
wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.
Wakampelekea Yezebeli habari,
wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya
kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka,
ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa
fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba
Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi
Myezreeli, ili alitamalaki.
Neno la Bwana... Tumshukuru
Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 5:2-3, 5-7 (K) 2
(K) Uisikie sauti ya kilio
changu, ee Bwana.
Uisikie sauti ya kilio changu,
Ee Mfalme wangu na Mungu wangu,
Kwa maana Wewe ndiwe
nikuombaye.
Bwana, asubuhi utaisikia sauti
yangu,
Asubuhi nitakupangia dua yangu
na kutazamia. (K)
Wajivunao hawatasimama mbele za
macho yako;
Unawachukia wote watendao
ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye
hila. (K)
Bali mimi, kwa wingi wa fadhili
zako,
Na kusujudu kwa kicho,
Nikielekea hekalu lako
takatifu. (K)
SHANGILIO
Kol. 3:16, 17
Aleluya, aleluya,
Neno la Kristu likae kwa wingi
ndani yenu katika hekima yote;
Mkimshukuru Mungu Baba kwa
Yeye.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:38 – 42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake:
Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi
nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume,
mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie
na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.
Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2026, "MASOMO
YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:
Post a Comment