Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 30, 2023


MASOMO YA MISA, MEI 30, 2023
JUMANNE JUMA LA 8 LA MWAKA

SOMO 1
YbS. 35 : 1-12

Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani; amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora; naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabihu ya kushukuru. Kuuacha uovu kwampendeza Bwana, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho. Lakini ujihadhari usitokee mbele za Bwana mikono mitupu; maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri. Toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu tamu yake yafika mbele zake Aliye juu. Dhabihu ya mwenye haki yakubalikana, wala kumbukumbu lake halisahauliki. Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe; na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu. Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba. Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Bwana ndiya mhukumu wala hakijali cheo cha mtu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 50 : 5-8, 14, 23

(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu autengenezaye mwenendo wake.

Nikusanyieni wacha Mungu wangu
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.


Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena,
Mimi nitakushuhudia, Israeli;
Mimi ndimi niliye Mungu, Mungu wako.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu autengenezaye mwenendo wake.

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru,
Mtimizie Aliye iuu nadhiri zako.
Atoaye dhabihu za kushukuru,
Ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.



SHANGILIO 
Lk 8:15
Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu.
Aleluya.


INJILI
Mk. 10:28-31

Petro alimwambia Yesu, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati   huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na. mama, na watoto na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza. 

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment