MASOMO YA MISA, MEI 9, 2024
JUMA LA 6 LA PASAKA, ALHAMISI
SOMO 1
Mdo. 18 :1-8
Siku zile, Paulo alitoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzaliwa wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.
Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98: 1-4 (K) 2
(K) Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa: au: Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
SHANGILIO
Lk 24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.
INJILI
Yn. 16: 16-20
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba? Basi walisema, neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo.
Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment