Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MACHI 3, 2024


MASOMO YA MISA, MACHI 3, 2024
JUMAPILI YA 3 YA KWARESIMA


MWANZO:
Za. 25:15-16

Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye akanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa.


SOMO 1
Kut. 20:1-17

Mungu alinena maneno haya yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu ila mimi.

Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.

Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.

Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya sabato akaitakasa.

Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala chochote alicho nacho jirani yako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:7-10 (K) Yn. 6:69

(K) Wewe, Bwana, ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima. (K)

Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)

Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)

Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali. (K)


SOMO 2
1Kor. 1:22-25

Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuuzi; bali kwao waitwao, WAyahudi kwa WAyunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima Zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu Zaidi ya wanadamu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Yn. 3:16

Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.


INJILI
Yn. 2:13-25

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. 

Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya?

Yesu akajibu, akwaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.

Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?

Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.

Hata alipkuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizofanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment