Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA DESEMBA 14, 2022


MASOMO YA MISA DESEMBA 14, 2022
JUMATANO, JUMA LA 3 LA MAJILIO 

KUMBUKUMBU YA MT. YOHANE WA MSALABA, 
PADRE NA MWALIMU WA KANISA

SOMO 1
Isa 45:6-8, 18-25

Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kuihuluku giza; mimi nafanya suluhu na kuhuluku ubaya; mimi ni Bwana niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu yamwage haki; nchi na ifunuke ili kutoa wokovu, nayo itoe haki ikemee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba. Maana Bwana aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, Mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia. Kwa Bwana, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkadirikia watatahayarika. Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab 85 :8a, 9-13


(K) Dondokeni, enyi mbingu, toka juu,
Mawingu na yamwage haki.

1.Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)

2.Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana,
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3.Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)


SHANGILIO
Isa. 45:8

Aleluya, aleluya,
Dondokeni, enyi mbingu toka juu, Mawingu yamwage haki; nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu.
Aleluya.


INJILI
Lk 7:19-23

Siku ile Yohane aliwaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu, akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohane Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa Habari Njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Krist0.


Copyright © 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment