“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatano, Desemba 14, 2022
Juma la 3 la Majilio
Kumbukumbu ya Mt. Yohane wa Msalaba, Padre na
Mwalimu wa Kanisa
Isa 45: 6-8, 18-25;
Zab 85: 8, 9-13;
Lk 7: 19-23.
JE, NI YESU UNAMSUBIRIA?
Katika Injili ya Luka leo, Yohane Mbatizaji
anawaagiza Wafuasi wamuulize Yesu, “Je, ni yeye ajaye au tumtazamie mwingine?”
Hili pia ni swali la muhimu sana lililopo ndani kabisa mwa moyo wa kila mmoja
wetu, je ni ‘wewe’ ninayekusubiri, ‘ambaye’ nimekusubiri maisha yangu yote? Na
Yesu anakuwa nashauku ya kumjibu Yohane na sisi pia, Yesu anatoa jibu hili:
“Nendeni mkamwambie Yohane mliyo yaona ninyi na kusikia, vipofu wanapona,
viwete wanatembea, wakoma wanaponywa, viziwi wanapata kusikia na waliokufa
wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema”. Kwa maneno mengine, Yesu
anatujibu sisi akisema,”mimi ndiye unayemsubiri, ambaye amekuja kukuokoa na
kufanya mambo yote mapya”
Injili hii inatualika tuyaseme maswali yetu
yaliyo ndani kabisa mwa mioyo yetu, na kwa nguvu kabisa ya unyenyekevu kama wa
Yohane, tumuulize Yesu kilichopo ndani kabisa mwa mioyo yetu. Yesu anatamani
kututimizia hamu ya mioyo yetu, atafanya hivyo tuu kama sisi tutaonesha
unyenyekevu wa kumwomba, kwasababu Yesu haingilii uhuru wa mwanadamu. Ni jukumu
letu tuchague lililo sahihi tutumie uhuru wetu vizuri na kumwomba yeye, kwani
kwa hakika yupo tayari kutimiza tunayotaka kumwomba.
Tunaomba kipindi hiki cha Majilio kiwe kipindi
cha kumtambua Yesu, ukweli, ambao tunautafuta. Tuzamishe mawazo yetu kwake
tuweze kusikia yale yote anayotaka kutuambia Bwana wetu.
Sala: Bwana, nisaidie katika kipindi hiki cha
majilio kuendelea kuandaa moyo wangu. Nisaidie nisikie maneno yako na yote
unayotaka kusema nami. Naomba nikufuate katika yote na kati ya yote nikutambue
wewe kama Mwokozi wa maisha yangu, Mkombozi ambaye nimemsubiria katika maisha
yangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment