MASOMO YA MISA, NOVEMBA
1, 2023
JUMATANO, JUMA LA 30 LA
MWAKA
SHEREHE YA WATAKATIFU
WOTE
_____________
SOMO 1
Ufu. 7:2-4,9-14
Mimi Yohane, niliona
malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye
hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi
na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha
kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia
hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na
arobaini na nne elfu.
Baada ya hayo nikaona,
na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila
taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi,
na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende
mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye
katika kiti cha enzi, na Mwana-kondoo.
Na malaika wote walikuwa
wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye
uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu
Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na
uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa
wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa aliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao
wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio
wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe
katika damu ya Mwana-kondoo.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu
_____________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 24:1-6 (K) 6
(K) Hiki ndicho kizazi
cha wakutafutao, Ee Bwana.
Nchi na vyote viijazavyo
ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao
ndani yake.
Maana ameiweka misingi
yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji
aliithibitisha. (K)
Ni nani atakayepanda
katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama
katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi
na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake
kwa ubatili. (K)
Atapokea Baraka kwa
Bwana,
Na haki kwa Mungu wa
wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha
wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee
Mungu wa Yakobo. (K)
_____________
SOMO 2
1 Yoh. 3:1-3
Tazameni, ni pendo la
namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa
sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu
wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa
atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila
mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa; kama yeye alivyo mtakatifu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu
_____________
SHANGILIO
Mt. 11:28
Aleuya, aleluya.
Njoni kwangu, ninyi
nyote msumbukao na wenye kulemewa
na mizigo, nami
nitawapumzisha, asema Bwana.
Aleluya.
_____________
INJILI
Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona
makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjua;
akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
Heri walio maskini wa
roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri wenye huzuni; Maana
hao watafarijika.
Heri wenye upole; Maana
hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu
ya haki; Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema; Maana
hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi;
Maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi; Maana
hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa
ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi
watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili
yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa
maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
_____________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment