Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA OKTOBA 4, 2023


MASOMO YA MISA OKTOBA 4, 2023
JUMATANO JUMA LA 26 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MT. FRANSISKO WA ASIZI
________

SOMO 1
Neh. 2:1-8

Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Name mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wowote. Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana. Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto? Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba?
Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga. Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.
Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda; nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu
________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 137:1-6

(K) Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa la kinywa change, nisipokukumbuka.

Kando ya mito ya Babeli ndipo tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu. (K)

Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka furaha;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. (K)

Tuimbeje wimbo wa Bwana
Katika nchi ya ugeni?
Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,
Mkono wangu wa kuume na usahau. (K)

Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa change, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)
________

SHANGILIO
Zab. 147:12

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
________

INJILI
Lk. 9:57-62

Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata kokote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake.
Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia, Waache wafu wawazike wafu; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu.
Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusu kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________

Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.


No comments:

Post a Comment