MASOMO YA MISA, OKTOBA
3, 2023
JUMANNE, JUMA LA 26 LA
MWAKA
SOMO 1
Zek. 8:20-23
Bwana wa majeshi asema
hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi;
wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni zetu kwa haraka
tuombe fadhili za Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi nami nitakwenda. Naam,
watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa
majeshi, na kuomba fadhili za Bwana.
Bwana wa majeshi asema
hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo
yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi,
kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 87 (K) Zek. 8:23
(K) Mungu yu pamoja
nasi.
Msingi wake upo
Juu ya milima
mitakatifu.
Bwana ayapenda malango
ya Sayuni
Kuliko maskani zote za
Yakobo.
Umetajwa kwa mambo
matukufu,
Ee Mji wa Mungu. (K)
Nitataja Rahabu na
Babeli
Miongoni mwao
wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro,
na Kushi;
Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni
itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa
humo. (K)
Na Yeye Aliye juu
Ataufanya imara.
Bwana atahesabu,
awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na
waseme,
Visiwa vyangu vyote vimo
mwako. (K)
________
SHANGILIO
Zab. 119:105
Aleluya, Aleluya,
Neno lako ni taa ya
miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 9:51 – 56
Ilikuwa, siku za kupaa
kwake zilipokuwa karibu kutimia, Yesu aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;
akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji
cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa
vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohane
walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni,
uwaangamize? Akawageukia akawakanya, wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment