MASOMO YA MISA OKTOBA
25, 2023
JUMATANO, JUMA LA 29 LA
MWAKA
SOMO 1
Rum. 6:12-18
Dhambi isitawale ndani
ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee
kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe
kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za
haki. Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria,
bali chini ya neema.
Ni nini basi? Tufanye
dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha! Hamjui ya
kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii,
mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa utii uletao mauti,
au kwa mba ni utumishi wa utii uletao haki. Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa
maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu
ambayo mliwekwa chini yake; na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi mkawa
watumwa wa haki.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
_____________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 124 (K)
(K) Msaada wetu u katika
jina la Bwana.
Kama si Bwana aliyekuwa
pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa
pamoja nasi,
Wanadamu
walipotushambulia.
Papo hapo wangalitumeza
hai,
Hasira yao ilipowaka juu
yetu. (K)
Papo hapo maji
yangalitudharikisha,
Mto ungalipita juu ya
roho zetu;
Papo hapo yangalipita
juu ya nafsi zetu,
Maji yafurikayo.
Na ahimidiwe Bwana;
Asiyetutoa kuwa mawindo
kwa meno yao. (K)
Nafsi yetu imeokoka kama
ndege,
Katika mtego wa
wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi
tumeokoka.
Msaada wetu u katika
jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu na
nchi. (K)
_____________
SHANGILIO
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Mimi
ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
_____________
INJILI
Lk. 12:39-48
Yesu aliwaambia
wanafunzi wake: Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa
atakayokuja mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi
jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.
Petro akamwambia, Bwana,
mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani,
basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya
utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye
bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu
vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia
kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na
kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua,
atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini.
Na mtumwa yule aliyejua
mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa
sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na
kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi,
kwake huyo watataka na zaidi.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo
_____________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.
Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment