
“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Septemba 8, 2025
Juma la 23 la Mwaka
Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria
Mik 5: 1-4 au Rum 8: 28-30;
Zab 12: 6;
Mt 1: 1-16, 18-23
MUNGU ANA MPANGO NASI!
Bikira Maria Mama yetu, alichukuliwa mimba kitakatifu, alizaliwa na kuishi
bila dhambi, na sasa anatuombea ili hata mmoja wetu asipotee. Sisi, wanawe
tunafurahi kusheherekea sikukuu yake ya kuzaliwa. Kuhusu sikukuu ya leo Mt.
Andrea wa Crete anasema,"viumbe vyote vilivyo umbwa viimbe sifa na kucheza
na kwa pamoja viungane kuadhimisha utukufu wa siku hii...kwani leo hekalu
limejengwa kwa ajili ya Muumba wa ulimwengu". Maria alizaliwa kama hekalu
la Muumba, na kwa njia ya utii wake akatimiza lengo lake ambalo alizaliwa kwa
ajili yalo.
Kama Mungu alivyokuwa na mpango kwa Maria, kuzaliwa kwetu sio kwa bahati
mbaya au makosa. Mungu ana mpango nasi. Kama Maria alivyotimiza lengo lake
duniani, tunapaswa kutambua lengo letu katika maisha na kuwa waaminifu kwa
lengo hilo. Tunapaswa kuheshimu maisha ya wengine pia, kwani Mungu naye ana
mpango nao pia! Tuwaombee kwa namna ya pekee “ watoto wa kike” ambao siku hii
pia ni maalumu kwa ajili yao pia
Sala: Salamu Maria uliye jaa neema Bwana yu nawe umebarikiwa kuliko
wanawake wote na Yesu mzawa wa tumbo lako amebarikiwa, Maria Mtakatifu Mama wa
Mungu tuombee sisi wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
No comments:
Post a Comment