MASOMO YA MISA, ALHAMISI, SEPTEMBA 4, 2025
JUMA LA 22 LA MWAKA
SOMO 1
Kol. 1:9-14
Tangu siku tuliposikia habari yenu, hatuachi
kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika
hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana,
mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika
maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu
wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha;
mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu
katika nuru.
Naye alituokoa katika nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika
yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:2-6 (K) 2
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K)
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za mfalme, Bwana. (K)
________
SHAGILIO
1Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo
ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 5:1 – 11
Makutano walipomsonga Yesu wakilisikiliza neno
la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo
viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.
Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke kidogo
na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.
Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni,
Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simony akajibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate
kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata
samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika
wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza
vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.
Simoni Petro alipona hayo, alianguka magotini pa
yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana
alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi
wa samaki walaioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo,
waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa
utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha
vyote wakamfuata.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
🙏🏽
ReplyDelete