MASOMO YA MISA, SEPTEMBA
30, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 25 LA
MWAKA
SOMO 1
Zek. 2:1-5, 10-11
Niliinua macho yangu,
nikaona, na tazama, mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake. Ndipo nikasema,
unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake
ulivyo na urefu wake ulivyo. Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu,
na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye; naye akamwambia, Piga mbio,
kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji
visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake. Kwa
maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami
nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakaa, kati yako, asema
Bwana. Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu
wangu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. Yer. 31:10-13
(K) Bwana atatulinda
kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Lisikieni neno la Bwana,
enyi mataifa,
Litangazeni visiwani
mbali, mkaseme,
Aliyemtawanya Israeli
atamkusanya,
Na kumlinda kama
mchungaji alindavyo kundi lake. (K)
Kwa maana Bwana amemweka
huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake
aliyekuwa hodari kuliko
yeye. (K)
nao watakuja, na kuimba
katika mlima Sayuni,
wataukimbilia wema wa
Bwana,
nafaka, na divai, na
mafuta,
na wachanga wa kondoo na
wa ng’ombe.
Na roho zao zitakuwa
kama bustani iliyotiwa maji,
Wala hawatahuzunika tena
kabisa. (K)
Ndipo bikira atafurahi
katika kucheza,
Na vijana na wazee
pamoja.
Maana nitageuza
masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na
kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)
________
SHANGILIO
Zab. 119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu
niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 9:34 – 45
Makutano walipokuwa
wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake,
Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa
katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao
wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2017,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment