MASOMO YA MISA, SEPTEMBA
27, 2023
JUMATANO, JUMA LA 25 LA
MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT.
VINSENTI WA PAULO
SOMO 1
Ezr. 9:5-9
Wakati wa sadaka ya jioni, mimi Ezra niliinuka
baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka
magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu wangu; nikasema, Ee
Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu;
kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu
imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia
kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani
wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga,
tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama
hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu, hata
akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu
wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu. Maana
sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali
ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha,
tuisimamishe nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta
katika Yuda na Yerusalemu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Tob. 13:2-4, 6 (K) 1
(K) Amehimidiwa Mungu
aishiye milele.
Kwa maana hurudi, na kurehemu tena;
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K)
Enyi bani Israeli, mshukuruni mbele ya mataifa
Yeye ambaye ametutawanya katikati yao. (K)
Kuko huko utangazeni ukuu wake,
Mwadhimisheni mbele ya wote walio hai;
Kwa kuwa Yeye ndiye Bwana wetu,
Naye Mungu yu Baba wetu,
Naye Mungu yu Baba yetu milele. (K)
________
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana.
Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 9:1-6
Yesu aliwaita wale Thenashara, akawapa uwezo na
mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa
Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo,
wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na
nyumba yoyote mtakayoingia kaeni humo, tokeni humo. Na wale wasiowakaribisha,
mtokakpo katika mji huo yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa
ushuhuda juu yao. Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri Injili, na
kupoza watu kila mahali.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment