MASOMO YA MISA, SEPTEMBA
26, 2023
JUMANNE, JUMA LA 25 LA
MWAKA
SOMO 1
Ezr. 6:7-8, 12, 14-20
Mfalme Dario alimwandikia liwali wa ng’ambo wa
mto, na wenzake; Waacheni liwali wa Wayahudi na wazee wa Wayahudi, waijenge
nyumba hii ya Mungu mahali pake. Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi
mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu;
katika mali ya mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng’ambo ya Mto, watu
hao wapewe gharama zote kwa bidii, ili wasizuiliwe. Na Mungu huyu, aliyelifanya
jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakonyosha
mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko
Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi. Nao wazee
wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa masaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii,
na Zekaria mwana wa Ido.
Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya
Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa
Uajemi. Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa
sita wa kutawala kwake mfalme Dario. Na wana wa Israeli, na makuhani, na walawi
na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfru nyumba ya Mungu kwa
furaha. Na katika kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng’ombe mia,
na kondoo waume mia mbili, na wanakondoo mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi
na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote, kwa hesabu ya
kabila za Israeli. Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi
vilivyoandikwa katika chuo cha Musa. Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka,
mwezi wa kwanza, siku ya kumi nan ne ya mwezi. Kwa maana makuhani na Walawi
walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja
pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani,
na kwa ajili ya nafsi zao.
Neno la Bwana… Tumshukuru
Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 122:1-5 (K) 1
(K) Nalifurahi
waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana. (K)
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu!
Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana. (K)
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana;
Ushuhuda wa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
________
SHANGILIO
1Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo
ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 8:19 – 21
Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake,
wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, Mama
yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. Akawajibu akasema,
Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment