“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Septemba 26, 2023
Juma la 25 la Mwaka
Ezra 6: 7-8,12,14-20;
Zab 121: 1-5;
Lk 8: 19-21
FAMILIA YA MUNGU!
Familia changa kwa kawaida inaonekana kuwa na umoja na mshikamono zaidi kwa
mtazamo wa hapa duniani. Lakini, Yesu anatufundisha kwamba kuna uhusiano na
umoja wa karibu zaidi kuliko wa familia, umoja na mshikamano alio nao kati yake
na wafuasi wake. Hili ndilo fundisho tunalo pata kutoka katika Injili ya leo.
Yesu alikuwa amesimama mbele ya umati wa watu akiwafundisha na mara moja ukaja
ujumbe, kwamba Mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje wakitaka
kumuona. Jibu lake kwao linaonekana kama anamkataa Mama yake. Haikatai familia
yake na wala hakuonesha kwamba haina umuhimu, na wala hakufundisha kwamba
familia ya Kibinadamu ina nafasi ndogo kwa Mungu. Yeye anatangaza kuhusu uwepo
wa familia ya pekee-familia ya kiroho. Familia ya kiroho na uhusiano wake
umejikita katika Neno la Mungu-kulisikia na kuliishi. Mtu aliye karibu na Mungu
ni mtu anaye mtii Mungu, anaye chukulia neno lake kwa umakini.
Yesu anasema wale wanao lishika neno lake na kuliishi ndio Mama, Kaka na
ndugu zake. Bikira Maria Mama yake, ndiye wakwanza kabisa kulisikia neno la
Mungu na kulitenda katika ukamilifu wote, kwa hiyo unaweza kuona kwamba Yesu
hakumkataa Mama yake bali alitaka sisi nasi tuwe ndugu zake kwa kuishi katika
kulishika neno lake. Sisi tutakuwa ndugu wa Yesu kweli kama tutaishi kadiri ya
Mafundisho yake. Tunaweza kusema tunampenda Yesu kweli kama tunashika yale
aliyo tufundisha. Tusizibe masikio yetu kwa wenzetu wala kwa maskini wanapo
kuwa na shida kwasababu sisi tunakuwa familia moja na Yesu na wala tusitamani
uovu kwasababu kiongozi wetu hana uovu ndani yake.
Tutafakari leo kuhusu mwaliko wa Yesu wa kututaka sisi tuweze kuwa mmoja
wapo wa familia yake, sema “ndio” kwa mwaliko huu. Tuwe tayari kwa sauti yake
na Umungu wake utabadilisha maisha yetu.
Sala: Bwana, ninapokea mwaliko wako wa kuwa mmoja wapo wa familia yako ya
karibu. Ninaomba nisikie sauti yako na niweze kutenda yale yote unayo niambia.
Yesu nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment