“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Septemba 15, 2025
Juma la 24 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu ya Bikira Maria Mtakatifu wa Mateso
Ebr 5: 7-9; au 1Kor 15:1-11
Zab 30: 2-6, 15-16, 20;
Yn 19: 25-27, 35 au Lk 2: 33-35
KUTESEKA KWA AMANI NA FURAHA!
Leo tunakumbuka mateso ya Mama yetu Bikira Maria. Mateso ya Maria yalikuwa
ya ndani. Bikira Maria alikuwa mwanadamu kamili kwasababu hakutenda dhambi na
kati ya watu waliompendeza Mungu katika hali ya ukamilifu wote ni Bikira Maria
licha ya Mwanae, lakini kwa ajili ya hili hatuwezi kusema hakuwa na hisia ya
kuhisi mambo ya duniani. Kwasababu ya ukamilifu wake, alipenda kwa mapendo ya
ndani kuliko sisi. Kwasababu ya upendo huu, alihisi uchungu wa kumpoteza mwanae
kuliko sisi. Mateso ya Maria tofauti na yetu yalikuwa kamili. Mateso yetu mara
nyingi yamechanganyika na udhaifu wetu. Maria hakuhuzunika kwasababu atamkosa
Mwanae ampe msaada. Aliteseka kwasababu aliona mateso ya yule anaye mpenda, na
akahisi mateso yale kama Mwanae alivyohisi. Tunaweza kuhisi pia ni kwa jinsi
ghani Yesu alivyojisikia alivyomuona Mamaye katika huzuni. Ni hakika
ilimsababishia mateso pia, lakini ilikuwa pia ni hali ya kuonesha ukaribu wao.
Ulimwengu mzima unaweza kuwa umekuwa wa ukatili na hali zote, lakini uso wa
Mama yake ulikuwa ni sehemu pekee alioweza kuelekezea macho yake, akiona sura
na mfano aliouweka wakati anatuumba sisi.
Huzuni ya mama haikuwa ni huzuni bila matumaini. Alijua kwa matumani fulani
kwamba Mwanae atafufuka kutoka wafu. Tumaini lake halikumzuia kuhisi uchungu na
wala halikumzuia kutazamia ufufuko wake. Maria ni Mama yetu. Kama ilivyo kwa
Mama mwema, anatufundisha sisi. Tunapaswa tutuoe muda wetu tukiwa naye katika
mti wa Msalaba, tukimuomba atufundishe jinsi ya kuhisi nasi mateso yetu katika
maisha. Tusisite kumkimbilia atuombee tunapokumbana na adha na mateso katika
maisha, yeye awe faraja na msaada wetu kwani atakuwa nasi, akisimama nasi na
kuteseka nasi, akiyaweka yote chini ya Msalaba wa Mwanae kwa niaba yetu.
Sala: Mama wa Upendo, Mama wa Mateso na Mama wa huruma, utuombee sisi.
Amina
No comments:
Post a Comment