Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, AGOSTI 8, 2025



MASOMO YA MISA, IJUMAA, AGOSTI 8, 2025
JUMA LA 18 LA MWAKA 

Kumbukumbu ya Mtakatifu Dominiko, Padre


SOMO 1
Kum 4: 32-40

Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pemhe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? Je! watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninvi katika Misri, mbele ya macho yenu?

Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto. Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi, ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nehi yao iwe urithi, kama ilivyo leo.

Kwa hivo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 77 :11-15, 20 (K) 11

(K) Ninayakumbuka matendo ya Bwana.

Nitayakumbuka matendo ya Bwana,
Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
Pia nitaitafakari kazi yako yote;
Nitaziwaza habari za matendo yako. (K)

Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu;
Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?
Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu;
Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa. (K)

Kwa mkono wako umewakomboa watu wako,
Wana wa Yakobo na Yusufu.
Uliwaongoza watu wako kama kundi,
Kwa mkono wa Musa na Haruni. (K)



SHANGILIO 
Mt. 4:4

Aleluya, aleluya, 
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. 
Aleluya.



INJILI
Mt. 16: 24-28

Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye vote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment