“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Juni 14, 2023
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 3: 4-11;
Zab 99: 5-9;
Mt 5: 17-19.
SHERIA YA UPENDO!
Katika Injili ya leo, Yesu kwa hakika anawahakikishia wanaomsikiliza
kwamba, “Sikuja kutengua sheria na manabii. Nimekuja si kutengua bali
kuikamilisha”. Yesu alikuja si kuifuta sheria bali aiinue katika hali ya juu ya
ukamilifu. Mtazamo wa Yesu unatusaidia tuione sheria katika mwanga mpya. Maneno
yake ni kwa ajili ya kufariji lakini pia yanaleta changamoto, akionesha njia
inayoenda juu sana kuliko sheria mpaka kwenye sheria ya Upendo. Sheria isiyo na
upendo haiwezi kulinda utu na maisha ya mwanadamu. Inamfanya mwanadamu awe kama
aina fulani ya kitu kisicho na uhai. Yesu anatutaka tuwe na upendo zaidi.
Pengine wakati mwingine tunasisitiza mno sheria kiasi cha kushindwa kuonesha
upendo na msamaha kwa wengine.
Tuwatazame watu walio wekwa na Mungu mbele yetu ili tuwapende. Hili ni kwa
ajili pia ya ndugu zetu katika familia lakini pia katika wana ndoa. Je, ni mara
ngapi tunavyokuwa makini kwa kitendo kidogo cha huruma na upendo?. Je
tunatafuta muda wa kutumia maneno ya kutia moyo? Je, tunatumia jitihada hata kuwaonesha
kwamba tunawajali? Upendo upo katika utukufu na utukufu huu unaonesha kushika
amri ya Mungu ya mapendo.
Katika maisha yetu, tunapaswa kuwa tayari kusonga mbele tukiwa wabunifu wa
njia mpya za kuweza kutufanya tuelewe na kuishi Imani yetu zaidi. Tamaduni zetu
na mapokeo yetu ni mazuri na tusiyapoteze lakini pia tutumie hali hiyo hiyo
katika kuelewa na kuangalia hitaji la sasa.
Sala: Bwana, nisaidie niweze kuwa makini kwa njia kubwa na katika njia
ndogo ndogo unazo niita ili kukupenda wewe na jirani. Nisaidie hasa, niweze
kuangalia muda hata mdogo nioneshe upendo na hivyo kutimiza sheria yako. Yesu
nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment