Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 14, 2023


MASOMO YA MISA, JUNI 14, 2023
JUMATANO, JUMA LA 10 LA MWAKA


SOMO 1
2Kor. 3:4 – 11

Tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu. Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko bali war oho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha. Basi, ikiwa huduma ya mauti iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi. Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana. Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 99:5 – 9 (K) 9

(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu;
Sujuduni penye kiti cha miguu yake;
Ndiye mtakatifu. (K)

Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake,
Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake,
Walipomwita Bwana aliwaitikia. (K)

Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao.
Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa. (K)

Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu;
Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe
Ingawa uliwapatiliza matendo yao. (K)

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu;
Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu;
Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu. (K)



SHANGILIO
Zab. 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.



INJILI
Mt. 5:17-19

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, mpaka mbingu nan chi zitakapoondoka, yodi moja wala nukata moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment