Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 25, 2023


MASOMO YA MISA, JUNI 25, 2023
JUMAPILI YA 12 YA MWAKA



SOMO 1
Yer. 20 : 10-13

Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo. nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; 
Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji 
Katika mikono ya watu watendao maovu.


Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 69 : 7-9, 13,16, 32-34 (K) 13

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.

Kwa ajili yako nimestahimili laumu,
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu yao wanaokulaumu zimenipata. (K)

Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, 
Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu,
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. (K)

Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yetu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu
Bahari na vyote viendavyo ndani yake. (K)



SOMO 2
Rum. 5:12-15

Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia uli mwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, alive mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.


Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.




SHANG1LIO
Mdo. 16:14

Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, ee Bwana, 
Ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.



INJILI
Mt. 10:26-33

Yesu aliwaambia mitume wake: Msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum, Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.


Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment