MASOMO YA MISA, JUNI 24, 2023
JUMAMOSI, JUMA L A 11 LA MWAKA
SHEREHE YA KUZALIWA MTAKATIFU YOHANE MBATIZAJI
SOMO 1
Isa 49:1-6
Nisikilizeni. enyi visiwa; tegeni masikio yenu.
enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni: toka tumbo
la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama
upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa
mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha.
Akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli,
ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema. Nimejitaabisha bure, nimetumia
nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu
yangu ina Mungu wangu.
Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu
tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena. na Israeli wakusanyike
mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu
wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi
wangu ili kuziinua kabila za Yakobo. na kuwarejeza watu wa Israeli
waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu
wangu hata miisho ya dunia.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 139:1-3, 13-15 (K) 14
(K) Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa.
Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote. (K)
Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K)
Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi
pande za chini za nchi. (K)
SOMO 2
Mdo. 13 : 22-26
Paulo alisema, Mungu alimwinua Daudi awe mfalme
wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu
anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu
huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane
alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba,
kabla ya kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena,
Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma
yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake. Ndugu zangu, wana
wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la
wokovu huu limepelekwa.
SHANGILIO
Lk. 1:76
Aleluya, aleluya, Nawe, mtoto, utaitwa nabii
wake aliye juu. Utatangulia mbele za uso wa Bwana, umtengenezee njia zake.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:57-66, 30
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti
zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya
kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya
nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye
akajibu, akasema, La, sivyo; bali, ataitwa Yohane. Wakamwambia, Hapana mtu
katika jamaa" zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo
kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohane. Wakastaajabu
wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena
akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo
hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote
walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa na namna
gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Yule mtoto akakua,
akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa
Israeli.
Injili ya
Bwana........Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment