MASOMO YA MISA, JUNI 21, 2023
JUMATANO, JUMA LA 11 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. ALOIS GONZAGA (MTAWA)
SOMO 1
2 Kor. 9:6 – 11
Nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba;
apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia
moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye
atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili
ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila
tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yakaa milele.
Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate
uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya
haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao
Mungu shukrani kwa kazi yetu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 112:1 – 2, 4 – 9 (K) 1
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. (K)
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi
kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
INJILI
Mt. 6:1-6, 16 – 18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo
sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na
njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu
yao. Basli wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono
wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao
wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili
waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe
usalipo, ingia katika chumba cha ndani,
na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba
yako aonaye sirini atakujazi.
Tena mfungapo, msiwe kama wanfiki wenye uso wa
kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao; ili waonekane na watu kuwa nafunga,
Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake
mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba
yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment