“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Juni 12, 2023
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 1: 1-7;
Zab 34: 2-9;
Mt 5: 1-12
HERI WALIO…..!
Yesu leo anaanza mazungumzo yake kwa maneno ya pekee ya heri. Zipo heri
nane, kila moja ikianza kwa “heri walio..”. Yesu anatumia neno hili la heri
ambalo kwa Kigirini ni Makarios ambalo ndani yake halibebi tuu furaha bali
linabeba neno bahati nzuri ya kupata baraka maalumu. Kwahiyo tunaweza kusema,
“heri walio…” au “Wanabahati kweli walio….”
Ufalme wake ni ufalme uliojaa huruma na msamaha. Na kama tutakavyokuwa
tayari kuwasamehe wenzetu tutajikuta pia wenzetu wanatusamehe tunapo wakosea.
Katika sala ya Bwana, ambayo ni sala ya Ufalme, huwa tunaomba hili, “tusamehe
dhambi zetu kama na sisi tunavyo wasamehe waliotukosea”. Kwa kawaida ni vigumu
sana kwa wale walio katika ufalme huu kutokusamehe, wao kawaida ni wepesi
kusamehe na kukaribisha amani. Hii haimaanishi kwamba tuwatendee kila ubaya.
Haki pia lazima iwepo. Kupinga na kukataa uovu haina maana ya kuacha kusamehe
na kuponya vidonda vilivyo sababishwa na wengine.
Na huruma inayoeleweka katika nyanja ya kujali wengine ndio inayojenga
Ufalme huu ndani ya mtu. Mtu huyu sio kwamba anaona huruma kwa wanaoteseka tuu
bali anajua pia jinsi yakujiingiza katika matatizo ya wengine na kuhuzunika nao
katika hali yao. Hii ndio sifa aliokuwa nayo Yesu katika hali zote. Aliingia
katika maisha ya watu na kukaa nao na kuleta furaha na matumaini mapya.
Sala: nisaidie niweze kuwa mpole na mwenye huruma, maskini wa roho, mwenye
kuleta Amani na mtu mwenye kukubali mateso. Nisaidie mimi niweze kupokea kwa
shauku na kwa furaha ufalme wako. Yesu nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment