“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kila siku
Jumanne, Juni 13, 2023,
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 1: 18-22;
Zab 119: 129-133, 135;
Mt 5: 13-16
CHUMVI NA MWANGA
Yesu anawaambia Wafuasi wake: ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Ninyi ni mwanga
wa ulimwengu. Maneno haya ni utangulizi wa maneno ambayo Yesu atayasema katika
hutuba ya mlimani. Wafuasi wa Yesu wanatakiwa maneno ya Yesu yapenye ndani yao,
ya watawale na wayaishi.
Katika Agano la Kale, WaisraelI walipewa Amri kumi na Agano likafanywa kati
yao likiwataka waishi kitakatifu na kwa haki kama wanavyotakiwa na Agano. Je,
walitambua wao ni chumvi ya ulimwengu?. Walisisitiza sana kuhusu sheria, mpaka
wakaua ile roho. Yesu anaonesha hili kwa wafuasi wake kwakuwaambia, wema wao
usipozama ndani nakuushinda ule wa Walimu wa sheria na Mafarisayo, hawawezi
kuwa chumvi ya ulimwengu. Yesu aliwataka Wafuasi wake wawe chumvi ya ulimwengu,
si kwakusimama na kuonekana kama watakatifu machoni pa watu bali kwa maadili
mema na utu ambao umevishwa taji ya upendo kwa Mungu na kwa jirani. Kwa wema,
maadili na utu huu uliovishwa taji, na kungarishwa na Imani, matumaini na
mapendo, wakristo wanaalikwa kuwa mwanga wa Ulimwengu. Hawahitaji kujitangaza
kwamba wao ni Wakristu. Wataonesha kwamba wao ni Wakristo “kwanjia hii wote
watajua ya kuwa ninyi ni wafuasi wangu, kama mna pendana ninyi kwa ninyi” (Yn
13: 35).
Kama tunavyoweza kufikiri mlo bila chumvi, au kupotelea msituni wakati wa
usiku, tutatambua ni kitu ghani Yesu anatuambia. Kiasi kidogo cha chumvi au
kiasi kidogo cha mwanga kina badili kila kitu. Mt. Fransisko wa Assis
anatuambia giza lote la ulimwengu mzima haliwezi kuzima hata mwanga wa mshumaa
mmoja. Ulimwengu tunaoishi upo gizani katika hali mbali mbali. Mungu anatuita
mimi na wewe tuweze kuwa chumvi na mwanga na kuwaonesha watu njia. Mungu
anataka kungara kupitia wewe na mimi, na anakutaka wewe uangaze. Jukumu letu ni
kuwa wawazi.
Sala: Bwana, ninataka kutumiwa na wewe. Ninataka kuwa chumvi na mwanga.
Ninataka kufanya mabadiliko ulimwenguni. Ninajitoa kwako kwa huduma yako. Yesu,
ninakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment