“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumamosi, Aprili 20, 2024
Juma la 3 la Pasaka
Mdo 9: 31-42;
Zab 116: 12-17;
Yn 6: 60-69.
UNA MANENO YA UZIMA WA MILELE!
Yohane anataka kutuonesha kwamba Yesu ndiye anayetulisha chakula cha uzima
wa Kimungu, kwakutupa sisi maisha yake mwenyewe na mwili wake. Kula mkate na
samaki aliowapa Yesu ilikuwa rahisi lakini kusikiliza maneno yake ilikuwa
vigumu, baada ya haya Injili inasema wazi kwamba wafuasi wengi walimwacha na
wengine waliacha kuambatana naye. Lakini wakati Yesu alipowauliza wale kumi na
wawili, kama na wao wanataka kuondoka pia, Petro alijibu, “Bwana tuende kwa
nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele” Ndio, Petro anatambua japo kuwa si
kwahakika sana kipindi hicho, kwamba “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai
kitu”
Swali hili la Yesu kwa Mitume wake ni muhimu sana. Kwa kuwauliza wao moja
kwa moja, Yesu anawapa uhuru kamili wa kuchagua. Hawashinikizi kukubali au
kuamini alichokuwa amefundisha mara. Hili lilikuwa muhimu kwa sababu kwa kiasi
ambacho Yesu anatoa cha kuachia yote ni mwaliko wa kuwa na uhuru kamili, kwa
upande wa mitume, kwa mafundisho yake ya utukufu juu ya Ekaristi. Wapo huru
kabisa kukubali au kukataa. Ni uhuru huu utawafanya wazame katika Imani yao juu
ya Yesu.
Tutafakari leo, juu ya kujikabidhi kwetu kwa Yesu. Tupo huru kabisa
kumfuata yeye au kumkataa. Yesu hapendi tumchague na kumfuata nusu nusu. Maneno
ya Yesu yana nguvu, yana changamoto na yanahitaji sadaka. Anataka tumwamini
yeye na kumfuata kwa moyo wote na kujikabidhi kweli. Ni Yesu mwenyewe mwenye
maneno ya uzima wa milele na tunapaswa tukubali maneno yake na kuamini kwa
nguvu zetu zote.
Ni neno la Mungu kweli linalo tutakasa na kutuburudisha. Linatupa uzima;
kwahiyo kinachotupa uzima ni Neno la Mungu, kwani maneno anayosema Yesu ni roho
tena ni uzima. Jumuiya ya Wakristo kama tunavyosikia katika Somo la kwanza leo,
walijenga msingi wao juu ya uzima huu walioupokea kutoka kwa Yesu na faraja ya
Roho Mtakatifu. Sisi tuna uhai na uzima, ila uzima wetu na maisha yetu tuyaweke
ndani ya Bwana wa uzima Yesu Kristo mwenyewe. Ni maneno haya yenye uzima ya
Yesu yalioweza kumrudishia uzima Dorcasi kama tunavyosikia katika somo la
kwanza.
Sala: Bwana Yesu, ni wewe pekee ninaye kuchagua kukuamini na kukufuata.
Nisaidie nikumbatie yote uliyo fundisha na nisaidie kukuchagua kwa uhuru katika
maisha yangu ya kila siku. Yesu nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment