MASOMO YA MISA, APRILI 20, 2024
JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 9:31-42
Kanisa lilipata raha katika Uyahudi wote na
Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongoezeka katika kicho cha
Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote
akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake
Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro
akamwambia. Ainea, Yesu Kriso akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka. Na
watu waliokaa Lida na Sharani wakamwona, wakamgeukia Bwana.
Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake
Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa
matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata
walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa
karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma
watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu.
Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika,
wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na
kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja
nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga maogi, akaomba, kisha akaelekea yule
maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro
akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua, hata akiisha kuwaita wale
watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji
mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 116:12-17 (K) 12
(K) Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote
alionitendea?
Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake. (K)
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umenifungua vifungo vyangu.
Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)
SHANGILIO
Kol. 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:60:69
Siku ile, watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake
waliposikia maneno ya Yesu juu ya mkate wa uzima, walisema: Neno hili ni gumu,
ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi
wake wanalinung’unukia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza?
Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho
ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena
ni uzima.
Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasiomini.
Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani
atakayemsaliti. Akasema, kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu
awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi
miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma wasiandamane naye tena.
Basi Yesu akawambia wale Thenashara, Je! Ninyi
nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani?
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa
wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment