Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TANO, JUMANNE



NOVENA YA ROHO MTAKATIFU 
SIKU YA TANO, JUMANNE
ROHO MTAKATIFU ANAWATAKASA WAUMINI



Walio wa Mungu watafuata yaliyo ya Mungu, na walio wa dunia hufuata yaliyo ya dunia,. Ni mauti kutosheka na mambo yaliyo ya dunia. Uzima na faraja ya kweli hupatikana tu katika mambo ya Mungu.

Kwa nguvu zetu sisi wenyewe hatuwezi kutenda lolote jema. Kuweza kwetu kwatoka kwa Mungu, kwatoka kwa Yeye anayetupa kujua, kupenda na kutenda.

Mtu anapotenda dhambi, hawezi kuongoka ila kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ndiye anayempa mkosefu neema ya kutambua ubaya wa kosa lakena kuamua kuliacha. Ndiye anayempa pia mkosefu kutambua uzuri wa neema aliyoipoteza na kumrudishia neema hiyo. Ndiye anayempa nguvu za kuidumisha neema hiyo na kuiongeza.

Isitoshe, Roho Mtakatifu ndiye anayemuwezesha mtu kuwa na maendeleo katika fadhila na utakatifu. Ndiye anayemjalia imani iliyo msingi wa maisha ya kiKristu. Ndie anayetujalia akili ya kushika mafumbo ya dini yetu na kuishi imani yetu mpaka kufa.

Lakini imani peke yake haimtoshi mtu aokoke. Imani pasipo matendo haifai kitu; imani bila matendo imekufa (Yak 2:28) Roho Mtakatifu anamuwezesha mtu kumuamini Mungu na kumenda kuliko vitu vyote na kumpenda jirani kama kujipenda mwenyewe. Ndiyo maana Roho Mtakatifu huitwa chanzo cha matendo yetu yote yaliyo mema. Basi, tumuombe Roho Mtakatifu aitakase mioyo yetu sisi waumini wake, atuzidishie imani, atuwezeshe kutenda matendo yaliyojaa imani.

1. Ewe Roho Mtakatifu, utudumishie imani, uyatakase mawazo ya mioyo yetu yafuate daima maongozi yako na amri zako
W. Twakuomba utusikie

2. Uzigeuze nia zetu zipate kumuelekea daima Mungu
W. Twakuomba utusikie

3. Utuwezeshe kuelekea katika utakatifu na kutenda mema kwa imani siku zote za maisha yetu
W. Twakuomba utusikie

4. Utuzidishie imani matumaini na mapendo, tuweze kushika kwa moyo thabiti yale yote tunayofundishwa na kanisa lako takatifu
W. Twakuomba utusikie

5. Uiwashe mioyo yetu na moto wa mapendo yako, tupate kumpenda Mungu kweli na kumpenda jirani yetu pasipo unafiki.
W. Twakuomba utusikie

6. Utusaidie tuishi vema kwa imani na matumaini siku zote za maisha yetu
W. Twakuomba utusikie

7. Utujalie kudumisha mioyoni mwetu ile neema ya utakaso tuliyoipata mwanzo katika ubatizo wetu
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ee Mungu, mbele yako mioyo yetu i wazi; wewe wayajua yote, wala hakuna siri iliyofichika mbele yako. Uyatakase mawazo ya mioyo yetu kwa kutupelekea Roho Mtakatifu, ili tuweze kukupenda na kukutukuza kama inavyostahili. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu


W. Amina

No comments:

Post a Comment