NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA KWANZA, IJUMAA
ROHO MTAKATIFU ANATUFARIJI
Yesu alipokuwa akiagana na mitume wake, kabla ya
kupaa mbinguni, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu mpaka hapo watakapokuwa
wamempokea Roho Mtakatifu. Aliwaambia: “Wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni,
mtajazwa nguvu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika nchi
yote ya Yuda na Samaria, hata kwenye mipaka yote ya dunia.” (Mdo.1:8)
Waliendelea kusali pamoja toka hapo Yesu
alipopaa mbinguni mpaka siku ya Pentekoste. Waliomba Roho Mtakatifu awashukie,
awajaze na mapaji yake. Na baada ya siku tisa Roho Mtakatifu aliwashukia hao
kundi dogo nao wakawa chanzo cha Kanisa lililopata kuenea duniani kote.
Siku hizo tisa za kusali zinaitwa NOVENA; na
kila mwaka wakati huu, wakristu wakifuata mfano wa mitume, wanasali muda wa
siku tisa kabla ya Sikukuu ya Pentekoste. Wanamuomba Roho Mtakatifu awashukie,
awajaze nguvu na wingi wa mapaji yake.
Wakati huu wa NOVENA , Tunayo mengi ya kuliombea Kanisa na kujiombea
sisi wenyewe. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kusali vema na kuomba
yale yote tunayohitaji kwa maslahi yetu ya roho na mwili.
Na kama mtume Paulo alivyowaambia wale waKristo
wa kwanza, Roho Mtakatifu huja kutufatiji katika udhaifu wetu. Basi tumuombe
atufariji kwa sala hizi za NOVENA, Atuwezeshe kusali na kuomba inavyotupasa
kusali.
1. Ee Baba wa milele, tunakuomba umtume Roho Mtakatifu atushukie sisi taifa
lako awashe ndani yetu moto wa upendo wako.
W. Twakuomba utusikie.
2. Ee Baba mwema, tunakuomba utujalie faraja ya Roho Mtakatifu sisi wana
tulio katika dhiki na taabu nyingi mno hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
3. Ulijalie Kanisa lako mapaji ya Roho wako Mtakatifu, liweze kutekeleza
vema utume wake wa kuhudumia watu wote hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
4. Utujalie sisi kudumu katika NOVENA hii mpaka mwisho kama Maria na mitume
walivyodumu pamoja wakisali kabla ya Pentekoste ile ya kwanza.
W. Twakuomba utusikie.
5. Utujalie neema zote zinazohitajika ili tuweze kumshuhudia Kristu popote
kwa mwenendo na matendo yetu ya kila siku, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie
6. Uzijalie familia zote za wakristu neema na nguvu za Roho Mtakatifu
tupate kuendelea pasipo kuchoka katika sala na katika matendo mema siku zote.
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe Roho Mtakatifu, uwajalie vijana wetu moyo wa ujasiri, wapate
kulijenga kanisa lako na kueneza utawala wako katika jumuia zetu za Kikristu.
W. Twakuomba utusikie.
TUOMBE:
Ee Mungu, uliye muumba wa vitu vyote, tunakuomba utusikilize kwa wema sala zetu
sisi taifa lako, utuongoze sote tufuate siku zote utaratibu wa mapenzi yako;
naye Roho Mtakatifu atutegemeze mpaka mwisho wa novena hii. Tunaomba hayo kwa
njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
No comments:
Post a Comment