JUMANNE, JUMA 4 LA PASAKA
KUMBUKUMBU YA MT. ATANASI (Askofu)
SOMO 1
Mdo 11:19-26
Siku zile, wale waliotawanyika kwa sababu ya ile
dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na
Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya
hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na
Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana
ukawa pamoja nao; watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.
Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa
kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia.
Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote
waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho
Mtakatifu na Imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.
Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli;
hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima
wakausanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa
Wakristo kwanza hapo Antiokia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 87:1-7 (K) 117:1
(K) Enyi mataifa yote, msifuni Bwana.
Au Aleluya.
Msingi wake upo
Juu ya milima mitakatifu.
Bwana ayapenda malango ya Sayuni
Kuliko maskani zote za Yakobo.
Umetanjwa kwa mambo matukufu,
Ee Mji wa Mungu. (K)
Nitataja Rahabu na Babeli
Miongoni mwao wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi;
Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa humo. (K)
Na Yeye Aliye juu
Ataufanya imara.
Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na waseme,
Visima vyangu vyote vimo mwako. (K)
SHANGILIO
Lk. 24:25-26
Huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku;
ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa
Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha
nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi.
Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi
hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo
zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo
wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami
nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu
atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko
wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na
Baba tu umoja.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment